- mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezajia
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha habari
NAIBU Waziri wa Maji, Eng. Maryprisca Mahundi (Mb), ameahidi kumaliza tatizo la maji kwenye Tarafa ya Mtae, iliyopo katika Jimbo la Mlalo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, wilayani Lushoto, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani.
Akizungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika Kata ya Mbaru na Rangwi, Eng. Mahundi, alisema kwamba Wizara yake chini ya Waziri wa Maji, Mhe. Juma Awesso ina taarifa juu ya changamoto za maji zinazoikabili Tarafa ya Mtae hii ni kutokana na swali ambalo aliwahi kuulizwa bungeni na Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Mhe. Rashid Shangazi.
Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subra na kuwa na imani na serikali yao kwa sababu, walipotoka ni mbali kuliko wanapokwenda na kueleza kuwa kwa sasa watakuwa na mipango ya aina mbili kwenye kutatua tatizo la maji kwenye Tarafa ya Mtae, hususani Kata za Mbaru, Rangwi na Sunga.
Alisema kwamba kwa kuanzia wanaenda kuboresha mradi mkongwe wa ENGOMAKA ili uweze kufanya kazi, huku serikali ikienda kutafuta suluhisho la muda mrefu, ambapo kwa sasa kuna Msanifu Mshauri ambaye anafanya kazi ya kutafuta vyanzo vikubwa zaidi vya maji kwenye maeneo hayo ili waweze kutengeneza mradi mkubwa zaidi kwenye mwaka ujao wa fedha.
Eng. Mahundi ametoa maagizo kwa RUWASA Wilaya ya Lushoto, kuhakikisha hadi kufikia mwisho wa mwezi wa pili, wanakuwa tayari wametatua matatizo ya mradi wa ENGOMAKA, ili wananchi wapate maji kwa kipindi hiki wakati serikali ikienda kutafuta suluhisho la muda mrefu kwenye mwaka ujao wa fedha.
Aliongeza kusema kwamba serikali itamlipa shilingi milioni 100, Msanifu Mshauri kwa ajili ya kutafuta chanzo cha uhakika na kuutaka uongozi wa Bonde la Pangani kushirikiana na mtaalamu huyo ili kufanikisha upatikanaji wa chanzo cha uhakika ili kumaliza kabisa tatizo la maji Tarafa ya Mtae.
Lakini, Eng. Mahundi aliendelea kusema kwamba ikiwa kitakosekana chanzo cha uhakika basi, serikali italazimika kuchimba visima virefu lengo likiwa ni kumaliza kabisa changamoto ya maji Tarafa ya Mtae na kumtua Mama ndoo kichwani kwa vitendo.
Katika hatua nyingine; Wananchi wa Kata ya Lukozi, waliotanda barabarani walifanikiwa kusimamisha msafara wa Eng. Mahundi na kumuwasilishia kero yao ya maji, ambapo aliwaahidi kutatua changamoto hiyo huku akiwasihi kuendelea kutunza vyanzo vya maji.
MAGUZONI, 18 BARABARA YA HALMASHAURI, 21782 Lushoto,Tanga
Postal Address: P.O.BOX 32 Lushoto
Telephone: +255(027)2977216
Mobile: +255 755 723 374
Email: ded@lushotodc.go.tz
Hatimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.Haki zote zimeifadhiwa